1 Wakorintho 4:8-18 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Haya! Mmekwisha shiba! Mmekwisha kuwa matajiri! Mmekuwa wafalme bila ya sisi! Naam, laiti mngekuwa kweli watawala, ili nasi pia tutawale pamoja nanyi.

9. Nafikiri Mungu ametufanya sisi mitume tuwe watu wa mwisho kabisa, kama watu waliohukumiwa kuuawa, maana tumekuwa tamasha mbele ya ulimwengu wote, mbele ya malaika na watu.

10. Sisi ni wapumbavu kwa ajili ya Kristo, lakini nyinyi ni wenye busara katika kuungana na Kristo! Sisi ni dhaifu, nyinyi ni wenye nguvu. Nyinyi mnaheshimika, sisi tunadharauliwa.

11. Mpaka dakika hii, sisi tuna njaa na kiu, hatuna nguo, twapigwa makofi, hatuna malazi.

12. Tena twataabika na kufanya kazi kwa mikono yetu wenyewe. Tukitukanwa, tunawatakia baraka; tukidhulumiwa, tunavumilia;

13. tukisingiziwa, tunajibu kwa adabu. Mpaka sasa tumetendewa kama uchafu wa dunia; na kwa kila mtu sisi ni takataka!

14. Siandiki mambo haya kwa ajili ya kuwaaibisha nyinyi, bali kwa ajili ya kuwafundisheni watoto wangu wapenzi.

15. Maana hata kama mnao maelfu ya walezi katika maisha yenu ya Kikristo, baba yenu ni mmoja tu, kwani katika kuungana na Kristo mimi ndiye niliyewazaeni kwa kuihubiri Habari Njema.

16. Kwa hiyo, nawasihi: Fuateni mfano wangu.

17. Ndiyo maana nimemtuma Timotheo kwenu. Yeye ni mtoto wangu mpenzi na mwaminifu katika kuungana na Bwana. Atawakumbusheni njia ninayofuata katika kuungana na Kristo; njia ninayofundisha kila mahali katika makanisa yote.

18. Baadhi yenu wameanza kuwa na majivuno wakidhani kwamba sitakuja tena kwenu.

1 Wakorintho 4