1 Wakorintho 15:35-42 Biblia Habari Njema (BHN)

35. Lakini mtu anaweza kuuliza: “Wafu watafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?”

36. Hayo ni maswali ya kijinga! Ukipanda mbegu, isipokufa kwanza haitaota.

37. Unachopanda ni mbegu tu, labda ya ngano au nafaka nyingine, na si mmea mzima ambao hutokea baadaye.

38. Mungu huipa hiyo mbegu mwili anaoutaka mwenyewe; kila mbegu hupata mwili wake wa pekee.

39. Miili ya viumbe vyote si sawa. Miili ya binadamu ni ya namna moja, ya wanyama ni ya namna nyingine, ya ndege ni ya namna nyingine na miili ya samaki pia ni ya namna nyingine.

40. Iko miili ya mbinguni na miili ya duniani; uzuri wa miili ya mbinguni ni mwingine, na uzuri wa miili ya duniani ni mwingine.

41. Uko uzuri wa jua, wa mwezi na wa nyota; hata nyota nazo huhitilafiana kwa uzuri.

42. Ndivyo ilivyo kuhusu ufufuo wa wafu. Kama vile mbegu, mwili huzikwa ardhini ukiwa katika hali ya kuharibika, lakini hufufuliwa katika hali ya kutoharibika.

1 Wakorintho 15