1. Naye mfalme Hiramu wa Tiro, aliyekuwa rafiki ya Daudi, alipopata habari kwamba Solomoni amekuwa mfalme mahali pa baba yake, alituma watumishi kwake.
2. Ndipo Solomoni akampelekea Hiramu ujumbe huu:
3. “Wajua kwamba baba yangu Daudi hakuweza kumjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, hekalu la kumwabudia, kwa sababu ya kukumbana na vita vingi dhidi ya maadui wa nchi jirani mpaka hapo Mwenyezi-Mungu alipompatia ushindi.
4. Lakini sasa, Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, amenijalia amani pande zote. Sina adui wala taabu.
5. Basi, nimeamua kumjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, nyumba ya kumwabudia. Na hii ni sawa kabisa kama Mwenyezi-Mungu alivyomwahidi baba yangu akisema: ‘Mwanao ambaye nitamfanya aketi katika kiti chako cha enzi, atanijengea nyumba!’