1 Timotheo 5:10-23 Biblia Habari Njema (BHN)

10. na awe mwenye sifa nzuri: Aliyewalea watoto wake vizuri, aliyewakaribisha wageni nyumbani kwake, aliyewaosha miguu watu wa Mungu, aliyewasaidia watu wenye taabu, na aliyejitolea kufanya mambo mema.

11. Usiwaandikishe wajane vijana, kwani kama tamaa zao za maumbile zikizidi kuwa na nguvu zaidi kuliko kujitolea kwao kwa Kristo, watataka kuolewa tena,

12. na wataonekana kukosa uaminifu kuhusu ahadi yao ya pale awali.

13. Wajane kama hao huanza kupoteza wakati wao wakizurura nyumba hata nyumba; tena ubaya zaidi ni kwamba huanza kuwasengenya watu, na kujitia katika mambo ya watu wengine, huku wakisema mambo ambayo hawangepaswa kusema.

14. Kwa hiyo ningependelea wajane vijana waolewe, wapate watoto na kutunza nyumba zao ili maadui zetu wasipewe nafasi ya kusema mambo maovu juu yetu.

15. Kwa maana wajane wengine wamekwisha potoka na kumfuata Shetani.

16. Lakini kama mama Mkristo anao wajane katika jamaa yake, yeye anapaswa kuwatunza na si kuliachia kanisa mzigo huo, ili kanisa liweze kuwatunza wajane wale waliobaki peke yao kabisa.

17. Viongozi wa kanisa wanaowaongoza watu vizuri wanastahili kupata riziki maradufu, hasa wale wanaofanya bidii katika kuhubiri na kufundisha.

18. Maana Maandiko Matakatifu yasema: “Usimfunge ng'ombe kinywa anapopura nafaka,” na tena “Mfanyakazi astahili malipo yake.”

19. Usikubali kupokea mashtaka dhidi ya mzee yasipowakilishwa na mashahidi wawili au watatu.

20. Wale wanaotenda dhambi waonye hadharani, ili wengine wapate kuogopa.

21. Nakuamuru mbele ya Mungu, mbele ya Kristo Yesu na mbele ya malaika watakatifu, uyazingatie maagizo haya bila kuacha hata moja, wala kumpendelea mtu yeyote katika kila unachotenda.

22. Usiharakishe kumwekea mtu yeyote mikono kwa ajili ya kumtumikia Bwana. Usishiriki dhambi za wengine; jiweke katika hali safi.

23. Usinywe maji tu, bali unywe divai kidogo kwa ajili ya tumbo lako, kwani unaugua mara kwa mara.

1 Timotheo 5