1. Usimkemee mwanamume mzee, bali msihi kama vile angekuwa baba yako. Watendee vijana wa kiume kama ndugu zako,
2. wanawake wazee kama mama zako, na vijana wa kike kama dada zako, kwa usafi wote.
3. Waheshimu wanawake wajane walio wajane kweli.
4. Lakini mjane aliye na watoto au wajukuu, hao wanapaswa kujifunza kutimiza wajibu wao wa kidini kwa jamaa zao wenyewe na hivyo kuwalipa wazazi wao na wazee wao, kwani hilo ni jambo la kupendeza mbele ya Mungu.
5. Mwanamke mjane kweli, asiye na mtu wa kumsaidia, amemwekea Mungu tumaini lake na huendelea kusali na kumwomba msaada usiku na mchana.
6. Lakini mwanamke ambaye huishi maisha ya anasa, huyo amekufa, ingawa yu hai.
7. Wape maagizo haya, wasije wakawa na lawama.
8. Lakini kama mtu hawatunzi watu wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani kwake, basi, mtu huyo ameikana imani, na ni mbaya zaidi kuliko mtu asiyeamini.
9. Usimtie katika orodha ya wajane mjane yeyote ambaye hajatimiza miaka sitini. Tena awe amepata kuolewa mara moja tu,
10. na awe mwenye sifa nzuri: Aliyewalea watoto wake vizuri, aliyewakaribisha wageni nyumbani kwake, aliyewaosha miguu watu wa Mungu, aliyewasaidia watu wenye taabu, na aliyejitolea kufanya mambo mema.
11. Usiwaandikishe wajane vijana, kwani kama tamaa zao za maumbile zikizidi kuwa na nguvu zaidi kuliko kujitolea kwao kwa Kristo, watataka kuolewa tena,
12. na wataonekana kukosa uaminifu kuhusu ahadi yao ya pale awali.
13. Wajane kama hao huanza kupoteza wakati wao wakizurura nyumba hata nyumba; tena ubaya zaidi ni kwamba huanza kuwasengenya watu, na kujitia katika mambo ya watu wengine, huku wakisema mambo ambayo hawangepaswa kusema.
14. Kwa hiyo ningependelea wajane vijana waolewe, wapate watoto na kutunza nyumba zao ili maadui zetu wasipewe nafasi ya kusema mambo maovu juu yetu.
15. Kwa maana wajane wengine wamekwisha potoka na kumfuata Shetani.
16. Lakini kama mama Mkristo anao wajane katika jamaa yake, yeye anapaswa kuwatunza na si kuliachia kanisa mzigo huo, ili kanisa liweze kuwatunza wajane wale waliobaki peke yao kabisa.