12. Wale wasichana wakawajibu, “Ndiyo, yuko. Tena yuko mbele yenu; mkifanya haraka mtamkuta. Ameingia tu mjini leo, kwa sababu leo watu watatambika huko mlimani.
13. Mara mtakapoingia mjini, mtamkuta kabla hajaenda mahali pa ibada mlimani ili kula. Maana watu hawatakula mpaka kwanza yeye abariki tambiko. Baadaye wale walioalikwa watakula. Hivyo nendeni haraka; mtakutana naye mara.”
14. Hivyo Shauli na mtumishi wake walikwenda mjini. Walipokuwa wanaingia mjini, walimwona Samueli akitoka mjini, na anaelekea mahali pa juu.
15. Jana yake, kabla Shauli hajafika mjini hapo, Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwambia hivi Samueli:
16. “Kesho, wakati kama huu, nitakuletea mtu kutoka nchi ya kabila la Benyamini, nawe utampaka mafuta kuwa mtawala wa watu wangu Israeli. Yeye atawaokoa watu wangu kutoka kwa Wafilisti, kwani nimeyaona mateso ya watu wangu na kilio chao kimenifikia.”
17. Samueli alipomwona tu Shauli, Mwenyezi-Mungu alimwambia, “Huyu ndiye yule mtu niliyekuambia. Yeye ndiye atakayewatawala watu wangu.”
18. Hapo Shauli alimwendea Samueli aliyekuwa karibu na lango la mji na kumwuliza, “Nakuomba unioneshe nyumba ya mwonaji.”