8. Mwenyezi-Mungu akamwita Samueli kwa mara ya tatu. Samueli akaamka, akamwendea Eli na kumwambia, “Nimekuja, kwani umeniita.” Ndipo Eli alipotambua kuwa Mwenyezi-Mungu ndiye aliyemwita Samueli.
9. Kwa hiyo Eli akamwambia Samueli, “Nenda ukalale, na akikuita, mwambie hivi: ‘Sema, ee Mwenyezi-Mungu, kwani mimi mtumishi wako nasikiliza.’” Hivyo Samueli akarudi na kulala mahali pake.
10. Baadaye Mwenyezi-Mungu akaja na kusimama hapo, akamwita Samueli kama hapo awali, “Samueli! Samueli!” Samueli akasema, “Sema, kwani mimi mtumishi wako nasikiliza.”
11. Kisha, Mwenyezi-Mungu akamwambia Samueli, “Tazama, nataka kutenda jambo fulani katika Israeli ambalo kila atakayesikia, atashtuka kulisikia.
12. Siku hiyo, nitatimiza yale yote niliyosema tangu mwanzo hadi mwisho dhidi ya Eli kuhusu jamaa yake.