9. Naye Meshelemia alikuwa na wana na nduguze; watu wenye uwezo kumi na wanne.
10. Hosa mmojawapo wa wana wa Merari alikuwa na wana wanne: Shimri (aliyefanywa kiongozi na baba yake hata ingawa hakuwa mzaliwa wa kwanza),
11. Hilkia wa pili, Tebalia wa tatu na Zekaria wa nne. Wana wote wa Hosa pamoja na nduguze walikuwa kumi na watatu.
12. Mabawabu hao waligawanyika katika makundi kulingana na jamaa zao, nao pia walipangiwa kazi kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu kama wale Walawi wengine.
13. Kila jamaa, bila kujali wingi, ilipiga kura kuchagua lango watakalosimamia.
14. Kura ya kuchagua wa kulinda lango la mashariki ilimwangukia Shelemia. Walipiga kura pia kwa ajili ya mwanawe Zekaria, aliyekuwa mshauri mwenye busara, ikamwangukia kura ya lango la kaskazini.
15. Obed-edomu aliangukiwa na kura ya lango la kusini, na ya wanawe, ghala.
16. Shupimu na Hosa waliangukiwa na kura ya kulinda lango la magharibi kwenye lango la Shalekethi kwenye barabara ya juu. Ulinzi ulifanywa kwa zamu.